Ijumaa, 23 Septemba 2016

KWA NINI UNAAJIRIWA? SEHEMU YA 3

Jana tuliendelea kuangazia mada hii mhimu. Tuligusia na kuangalia sababu za mwajiri kwa nini anataka mfanyakazi, tuliona ni kwa lengo tu la kutimiza malengo yake kwa kujiongezea mikono zaidi ya miwili aliyonayo.Leo tena tuangazie kipengele kingine, karibu

2. Unaajiriwa uli ulipwe mshahara.
Lengo la kila binadamu kuajiriwa hapa Duniani, ni ili alipwe mshahara akiwa na maono ya kukidhi mahitaji yake ya kila siku. Ajira humpatia mtu ridhiki yake ambayo hutokana na anacholipwa kutokana na kazi anayoifanya. Mwajiriwa huyu hupangiwa malipo atakayopokea kutoka kwa mwajiri wake, hivyo hana uhuru wa kupanga alipwe kiasi gani! Mwajiri ndiye hupanga akulipe kiasi gani. Ukishindwa kukubaliana na malipo anayokupa, basi unahiari ya kuacha kazi ukatafute sehemu nyingine, yeye hata hawezi kuumia kwa sababu anaamini ataajiri mtu mwingine na yamkini atamlipa kiasi kidogo zaidi ya alichokusudia kukulipa wewe. Na hii ni kwa sababu mwajiri anaamini wanaotafuta ajira ni wengi na maisha kwa wengi ni magumu, hivyo wako radhi kufanya kazi hata kwa malipo kidogo yanayoweza kukidhi mahitaji ya kula tu. Na mwajiriwa hupata mapato yake kila baada ya mwezi mzima jambo ambalo ni baya sana kwa usitawi wa maisha ya binadamu anayetaka kuendelea. Mwajiri yeye huingiza kipato kila siku kupitia mwajiriwa wake, wakati mwajiriwa huingiza kipato kila mwezi kutoka kwa mwajiri wake.

Mwajiri anakulipa kiasi tu kidogo sana kutoka kwenye faida anayoipata, hata kama ukilipwa kiasi kikubwa- basi ujue faida ya mwajiri wako ni kubwa zaidi, na anakulipa tu ili uendelee kumfanyia kazi zake. Na ndiyo maana faida yake ikipungua sana anapunguza wafanyakazi ili kukidhi matakwa yake ya kuingiza zaidi.

Tukutane wakati mwingine
Ni mimi mwezeshaji wako
Ngusa J.

Jumatano, 21 Septemba 2016

KWA NINI UNAAJIRIWA? SEHEMU YA 2

Jana tulianza kuichambua kwa kifupi mada hii ya kwa nini unaajiriwa? kwa sehemu tulianza tu kama utangulizi. Lakini leo tutaanza uchambuzi wa kina kuhusu mada hii. Tutaichambua mada hii kwa kuangazia vipengele kadhaa ambavyo ndani yake vimegawanyika. Vipengele hivyo ni pamoja na;
1- Kwa nini mwajiri anataka mfanyakazi?
2- Unaajiriwa ili ulipwe mshahara
3- Matarajio kwenye kuajiriwa
4- Mafanikio yatokanayo na kuajiriwa
5- Changamoto/ubaya wa kubwetekea ajira
6- Jipange uondoke kwenye makucha makali ya ajira.

Ndugu msomaji wangu, yawezekana baadhi ya vipengele hapo juu vinakera na kuleta ukakasi, lakini nivumilie tu naamini mpaka mwisho wa mada hii utakuwa umenielewa. Fuatana nami tuchambue vipengele hivi

1-Kwa nini mwajiri anataka mfanyakazi?
Wanadamu wote Duniani tumejaliwa kuwa na mikono miwili tu ya kufanya kazi, hivyo mikono yetu hutulazimisha kufanya kazi moja tu kwa wakati mmoja kwa sababu mikono yetu inauwezo huo (kama wapo wanaoweza kufanya kazi mbili au zaidi kwa wakati mmoja, basi wamejaliwa) Lakini hata akili huzama zaidi kwenye kitu kimoja badala ya kufanya Vitu zaidi ya kimoja kwa wakati mmoja. Changamoto huja kwa baadhi ya watu ambao hufikia kiwango ambacho wana mikono miwili tu, lakini kazi ni nyingi za kumwingizia kipato na zote zinapaswa zifanyike kwa wakati mmoja ili kuongeza mapato yake zaidi. Swali linakuja ana mikono miwili tu, je, atafanyeje kazi zote hizi kwa wakati mmoja? Hapa ndipo mtu huamua kutafuta mikono mingine ya kumsaidia kutimiza malengo yake

Mikono mingine: Kwa lugha rahisi huamua kutafuta watu awaajiri ili watimize malengo yake ya kuingiza kipato. Kwa hiyo maana yake ni kuwa, Muajiriwa huitwa Mikono ya mwajiri wake, maana mwajiri ameamua kuongeza mikono ya kufanya kazi zake kwa kuwa yeye ana mikono miwili tu na haitoshi. kwa hiyo, mwajiriwa ni kiungo tu (mikono) cha mwajiri wake na wala si kiungo chake mwenyewe.

Kumsaidia kutimiza malengo yake: Mwajiri huajiri akiwa na malengo ya biashara, kampuni, tasisi, au shirika lake. Kwa hiyo waajiriwa wote wanafanya kazi kwa lengo la kutimiza malengo ya kampuni, tasisi au shirika ambalo humilikiwa na mwajiri. Na mwajiriwa yeyote akiingiza malengo yake kwenye taasisi hiyo hutimuliwa kazi maana ameenda kinyume na malengo ya mwajiri wake, hata kama ataruhusiwa kuingiza malengo yake- yatapokelewa kama ushauri tu, na yatakubaliwa iwapo tu yanafaida kwa kampuni/taasisi na si vinginevyo. Kwa hiyo mwajiriwa hufanya kazi kwa manufaa ya mwajiri wake tu hata kama analipwa kiasi gani, akilipwa zaidi maana yake mwajiri anaingiza faida kubwa zaidi. Kwa hiyo ajira ya kuajiriwa si kazi ya aliyeajiriwa, ni kazi ya mwajiri, ni mikono ya mwajiri. Hakuna haja ya kusema kazi yangu hii, hapana ni kazi ya mtu mwingine. Kuna haja ya kutafuta kazi yako na wewe ujiajiri na kisha uajiri. Kwa leo tunakomea hapa, tukutane tena kesho kwa kipengele kingine.

Ni mimi mwezeshaji wako
Ngusa J.
 

Jumanne, 20 Septemba 2016

KWA NINI UNAAJIRIWA?

Kila siku vyuo vinabuniwa, kuanzishwa, kusajiliwa, kudahili na kupokea wanafunzi. Wakati huo vyuo vingine kila mwaka vinaandaa na kufanya mahafali za kuwaaga wahitimu wao. Mfumo wetu wa Elimu unawalazimisha wahitumu hawa aidha kusubiria ajira za serikali au kuzunguka na bahasha maofisini ili wapate ajira. Wachache sana ambao husoma wakiwa na malengo ya kujiajiri. Hata wamalizapo chuo hupitia wakati mgumu sana kuzisaka ajira na hapo ndipo huja wazo la kujiajiri, lakini hawana mitaji-waanzie wapi? Lakini swali muhimu linakuja, KWA NINI UNAAJIRIWA?

Hapa ndipo tunaweza anza uchambuzi wa swali hili adimu. Jibu ni moja tu- Unaajiriwa ili ulipwe mshahara. hivyohivyo kinyume chake, unajiajiri ili ujilipe mshahara, unaajiri ili ulipe mshahara. Lakini mada yetu kwa sasa ni kwa nini unaajiliwa? Tukutane kesho kwa uchambuzi hapahapa mtandaoni.
Ni mimi mhamasishaji wako
Ngusa J.
+225757990751/+255625163596

TUHAMIENI KWENYE UJASIRIAMALI


Maisha mtaani yamezidi kuwa magumu kwa watu wengi. Kila mmoja anajaribu kujikomboa kivyake, wengine wanaungana, wengine wanatengana, wengine wanaanzisha biashara, wengine biashara zao zinakufa, wengine wana mitaji ila hawajui waiwekeze wapi? Wengine wanawazo la biashara (Bussines idea) lakini hawana mtaji na hawajui pa kuupata, wengine wanasubiri ajira za serikali, wengine wanatoka kwenye ajira za serikali wakilenga kujiajiri wenyewe, wengine wanaajiri, wengine wanafukuza wafanyakazi, wengine wanaendesha mikokoteni- Wote hawa lengo lao kuu ni moja tu, kupambana na umasikini. Lakini hebu tutafakari pamoja maswali haya matatu;

1.Kwa nini uajiliwe?
2.Kwa nini ujiajiri?
3.Kwa nini unaajiri?

Naamini maswali haya matatu ni muhimu sana kwa mtu yeyote aliyelenga kupambana na adui dhalimu umasikini. Team yetu imeamua kukufikia wewe mjasiriamali, unayetegemea kuwa mjasiriamali na unayewaza kutoka kwenye ujasiriamali. Tumeamua kukufikia kwa njia ya mtandao huu, tukushirikishe, utushirikishe pia. Tutakuletea mada nyingi sana zitakazokuzindua na kukufanya uweze kufikia malengo yako. Pia timu yetu itakuhudumia katika nyanja zote za ujasiriamali ikiwa ni pamoja na kukuandalia Business plan kwa ajili ya biashara yako. Stay tuned...
Ni mhamasishaji wako
Ngusa J.
+225757990751/+225625163596