Jana tulianza kuichambua kwa kifupi mada hii ya kwa nini unaajiriwa? kwa sehemu tulianza tu kama utangulizi. Lakini leo tutaanza uchambuzi wa kina kuhusu mada hii. Tutaichambua mada hii kwa kuangazia vipengele kadhaa ambavyo ndani yake vimegawanyika. Vipengele hivyo ni pamoja na;
1- Kwa nini mwajiri anataka mfanyakazi?
2- Unaajiriwa ili ulipwe mshahara
3- Matarajio kwenye kuajiriwa
4- Mafanikio yatokanayo na kuajiriwa
5- Changamoto/ubaya wa kubwetekea ajira
6- Jipange uondoke kwenye makucha makali ya ajira.
Ndugu msomaji wangu, yawezekana baadhi ya vipengele hapo juu vinakera na kuleta ukakasi, lakini nivumilie tu naamini mpaka mwisho wa mada hii utakuwa umenielewa. Fuatana nami tuchambue vipengele hivi
1-Kwa nini mwajiri anataka mfanyakazi?
Wanadamu wote Duniani tumejaliwa kuwa na mikono miwili tu ya kufanya kazi, hivyo mikono yetu hutulazimisha kufanya kazi moja tu kwa wakati mmoja kwa sababu mikono yetu inauwezo huo (kama wapo wanaoweza kufanya kazi mbili au zaidi kwa wakati mmoja, basi wamejaliwa) Lakini hata akili huzama zaidi kwenye kitu kimoja badala ya kufanya Vitu zaidi ya kimoja kwa wakati mmoja. Changamoto huja kwa baadhi ya watu ambao hufikia kiwango ambacho wana mikono miwili tu, lakini kazi ni nyingi za kumwingizia kipato na zote zinapaswa zifanyike kwa wakati mmoja ili kuongeza mapato yake zaidi. Swali linakuja ana mikono miwili tu, je, atafanyeje kazi zote hizi kwa wakati mmoja? Hapa ndipo mtu huamua kutafuta mikono mingine ya kumsaidia kutimiza malengo yake.
Mikono mingine: Kwa lugha rahisi huamua kutafuta watu awaajiri ili watimize malengo yake ya kuingiza kipato. Kwa hiyo maana yake ni kuwa, Muajiriwa huitwa Mikono ya mwajiri wake, maana mwajiri ameamua kuongeza mikono ya kufanya kazi zake kwa kuwa yeye ana mikono miwili tu na haitoshi. kwa hiyo, mwajiriwa ni kiungo tu (mikono) cha mwajiri wake na wala si kiungo chake mwenyewe.
Kumsaidia kutimiza malengo yake: Mwajiri huajiri akiwa na malengo ya biashara, kampuni, tasisi, au shirika lake. Kwa hiyo waajiriwa wote wanafanya kazi kwa lengo la kutimiza malengo ya kampuni, tasisi au shirika ambalo humilikiwa na mwajiri. Na mwajiriwa yeyote akiingiza malengo yake kwenye taasisi hiyo hutimuliwa kazi maana ameenda kinyume na malengo ya mwajiri wake, hata kama ataruhusiwa kuingiza malengo yake- yatapokelewa kama ushauri tu, na yatakubaliwa iwapo tu yanafaida kwa kampuni/taasisi na si vinginevyo. Kwa hiyo mwajiriwa hufanya kazi kwa manufaa ya mwajiri wake tu hata kama analipwa kiasi gani, akilipwa zaidi maana yake mwajiri anaingiza faida kubwa zaidi. Kwa hiyo ajira ya kuajiriwa si kazi ya aliyeajiriwa, ni kazi ya mwajiri, ni mikono ya mwajiri. Hakuna haja ya kusema kazi yangu hii, hapana ni kazi ya mtu mwingine. Kuna haja ya kutafuta kazi yako na wewe ujiajiri na kisha uajiri. Kwa leo tunakomea hapa, tukutane tena kesho kwa kipengele kingine.
Ni mimi mwezeshaji wako
Ngusa J.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni